BARAZA LA MITIHANI LAPANGUA MFUMO MZIMA WA KUPANGA MADARAJA YA UFAULU KIDATO CHA NNE NA TANO

Matokeo ya Mtihani wa Majaribio (Mock) kwa mtihani wa Kidato cha Nne
mwaka huu na Kidato cha Sita mwakani, yatachangia alama 10 za Alama
Edelevu (CA). Kwa utaratibu huu, matokeo ya mwisho ya mtahiniwa,
yatatokana na asilimia 30 ya Alama Endelevu na asilimia 70 ni mchango wa
Alama za Mtihani wa Taifa.
Asilimia 30 za Alama Endelevu, zitapatikana kutokana na mitihani
mbalimbali. Kwa Kidato cha Nne mwaka huu, alama hizo zitatokana na
matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha pili ambao utakuwa na alama
10, matokeo ya kidato cha tatu muhula wa kwanza na wa pili alama tano,
matokeo ya mtihani wa majaribio (mock) wa Kidato cha Nne ni alama 10 na
majaribio ya kazi alama tano. Utaratibu huu umetokana na viwango vipya
vya ufaulu, vilivyoainishwa na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA)
kwenye kitabu cha Mwongozo wa Matumizi ya Viwango vya Ufaulu na
utaratibu wa kutunuku matokeo ya kidato cha nne na sita. Kwa Kidato cha
Sita, zitatokana na matokeo ya mtihani wa Kidato cha Tano muhula wa
kwanza na pili alama 15, matokeo ya 'mock' alama 10 na kazi mradi
itakuwa ni alama tano.“Katika somo ambalo mtahiniwa hakufanyia Kazi za
majaribio, alama za matokeo ya Mitihani ya 'Mock' ya Kidato cha Nne na
Kidato cha Sita, itachangia alama 15 badala ya 10 zilizoainishwa,”
imefafanua sehemu ya mwongozo huo. Hata hivyo, katika Mtihani wa Kidato
cha Nne mwaka jana na Kidato cha Sita mwaka huu, mchanganuo wa alama 30
za Alama Endelevu ni alama 15 zinazotokana na matokeo ya mtihani wa
Taifa wa Kidato cha Pili, asilimia 10 ilitokana na maendeleo ya mitihani
ya kidato cha Tatu muhula wa Kwanza na Pili na matokeo ya muhula wa
Kwanza Kidato cha Nne na kazi za majaribio asilimia tano. Kwa Kidato cha
Sita, alama endelevu ni matokeo ya Kidato cha Tano kwa mihula yote
miwili ni alama 15, muhula wa kwanza wa Kidato cha Sita ni asilimia 10
na kazi za majaribio ni asilimia tano. Aidha, Baraza limebadili
utaratibu wa kupanga madaraja ya kufaulu, kutoka mfumo wa Pointi na kuwa
wa Wastani wa Alama za Mtahiniwa (GPA). Mfumo unaotumiwa sasa wa
pointi, huonesha wastani wa pointi alizopata mtahiniwa kwa masomo
aliyofaulu zaidi, na kupanga madaraja kuanzia la kwanza hadi la
nne. Madaraja ya mfumo wa GPA, hupangwa katika utaratibu wa Distinction,
Merit, Pass na Fail. Daraja la Distinction ni la ufaulu wa juu zaidi na
daraja Pass ni ufaulu wa chini. Mtahiniwa hutunukiwa madaraja A, B+, B,
C, D, E au F kutegemeana na ufaulu wake katika somo ambapo uzito wa
alama katika madaraja A = 5, B+= 4, B = 3, C=2, D = 1, E = 0.5 na F =
0. Mtahiniwa atahesabiwa kuwa amefaulu somo, endapo atapata Daraja D
ambayo ni sawa na uzito wa alama moja. Ukokotoaji wa jumla ya GPA ya
mtahiniwa hufanyika kwa kuzingatia masomo, ambayo mtahiniwa amefaulu
angalau kwa daraja D na kuendelea (D, C, B, B+ na A).
GPA anayopata mtahiniwa hutokana na wastani wa pointi alizopata katika
masomo saba aliyofanya vizuri zaidi kwa Mtihani wa Kidato cha Nne au
masomo matatu ya mchepuo kwa Mtihani wa Kidato cha Sita.
Aidha, GPA ya mtahiniwa huandikwa katika nafasi moja ya desimali ambapo
nafasi ya pili ya desimali hukadiriwa katika makumi yaliyokaribu.
Mfano, mtahiniwa mwenye GPA ya 3.15 itakuwa sawa na 3.2 na mtahiniwa
mwenye GPA ya 3.14 itakuwa sawa na 3.1. Muundo wa madaraja ya GPA kwa
kidato cha nne, Distinction ni 3.6-5.0, Merit 2.6 -3.5, Credit 1.6-2.5,
Pass 0.3-1.5, Fail 0.0-0.2 wakati Kidato cha sita ni Distinction
3.7-5.0, Merit 3.0-3.6, Credit 1.7-2.9, Pass 0.7-1.6, Fail 0.0-0.6.
No comments:
Post a Comment